Job 42

Sehemu Ya Tano

(Ayubu 42)

Ayubu Anamjibu Bwana

1Ndipo Ayubu akamjibu Bwana:
2 a“Ninajua ya kuwa unaweza kufanya mambo yote,
wala hakuna mpango wako unaoweza kuzuilika.

3 bUliuliza, ‘Ni nani huyu afichaye mashauri yangu bila maarifa?’
Hakika nilisema juu ya mambo niliyokuwa siyaelewi,
mambo ya ajabu mno kwangu mimi kuyajua.


4 c“Ulisema, ‘Sikiliza sasa, nami nitanena;
nitakuuliza swali, nawe yakupasa kunijibu.’

5 dMasikio yangu yalikuwa yamesikia habari zako,
lakini sasa macho yangu yamekuona.

6 eKwa hiyo najidharau mwenyewe,
na kutubu katika mavumbi na majivu.”

Mwisho: Marafiki Wa Ayubu Wanafedheheshwa

7 fBaada ya Bwana kusema mambo haya yote na Ayubu, akamwambia Elifazi Mtemani, “Nina hasira juu yako na juu ya rafiki zako wawili, kwa sababu hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu. 8 gBasi sasa chukueni mafahali saba na kondoo dume saba mkamwendee mtumishi wangu Ayubu nanyi mkatoe sadaka za kuteketezwa kwa ajili yenu wenyewe. Mtumishi wangu Ayubu ataomba kwa ajili yenu, nami nitayakubali maombi yake ili nisiwatendee sawasawa na upumbavu wenu. Ninyi hamkusema yaliyo sawa kwa habari yangu, kama alivyosema mtumishi wangu Ayubu.” 9 hKwa hiyo Elifazi Mtemani, Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi wakafanya kama Bwana alivyowaambia; naye Bwana akayakubali maombi ya Ayubu.

10 iBaada ya Ayubu kuwaombea rafiki zake, Bwana akamwondoa kwenye uteka, akamfanikisha tena naye akampa mara mbili ya vile alivyokuwa navyo hapo mwanzoni. 11 jNdipo ndugu zake wote waume kwa wake na kila mtu aliyemfahamu mwanzoni, wakaja wakala pamoja naye katika nyumba yake. Wakamfariji na kumtuliza moyo juu ya taabu yote Bwana aliyoileta juu yake, nao kila mmoja akampa kipande cha fedha na pete ya dhahabu.

12 k Bwana akaibariki sehemu ya mwisho ya maisha ya Ayubu kuliko ile ya kwanza. Alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, ngamia elfu sita, jozi za mafahali elfu moja, na punda wa kike elfu moja. 13Tena alikuwa na wana saba na binti watatu. 14Binti wa kwanza aliitwa Yemima, wa pili Kesia na wa tatu Keren-Hapuki. 15Hapakuwepo mahali popote katika nchi ile yote palipopatikana wanawake wazuri kama binti za Ayubu; naye baba yao akawapa urithi pamoja na ndugu zao.

16Baada ya hili Ayubu akaishi miaka 140; akawaona wanawe na wana wa wanawe hata kizazi cha nne. 17 lHivyo Ayubu akafa, akiwa mzee aliyekuwa ameshiba siku.
Copyright information for SwhKC